Elon Musk na Mark Zuckerberg wakubali kushindana kwenye pigano kizimbani

Marion Bosire
1 Min Read

Elon Musk na Mark Zuckerberg ambao ni wawekezaji wakuu katika teknolojia wamekubali kushindana kwenye pigano kizimbani.

Musk ambaye ni mmiliki wa mtandao wa Twitter alisema hayo kupitia ujumbe wa Twitter ambapo aliandika kwamba yuko tayari kupigana kizimbani na Zuckerberg, mmiliki wa kampuni ya Meta inayoendesha mitandao ya Facebook na Instagram.

Zuckerberg alipiga picha ujumbe wa Musk akaichapisha akimtaka ampe eneo la tukio hilo.

Musk alijibu kwamba watapigana katika eneo la Vegas Octagon. Eneo hilo hutumika kwa mashindano ya ubingwa wa mapigano ya UFC.

Musk aliendelea kuvutia wafuasi wake mtandaoni akisema ana mbinu fulani anayotumia kwenye mapigano iitayo “The Walrus” inayohusisha kulalia mpinzani wake kwenye pigano bila kufanya lolote. Alichapisha video fupi zinazoonyesha mbinu hiyo.

Bwanyenye huyo ambaye alianzisha changamoto hiyo alikiri kwamba huwa hafanyi mazoezi isipokuwa wakati anacheza na watoto wake ambao huwa anawabeba na kuwarusha hewani.

Zuckerberg kwa upande wake hufanya mazoezi na amewahi kushinda taji kadhaa za mashindano ya mbinu za kujilinda kwenye mapigano almaarufu jiu-jitsu.

Majibizano ya matajiri hao wawili mitandaoni yamesababisha minong’ono kati ya watumizi wa mitandao ya kijamii huku wengine wakikisia mshindi wa shindano hilo.

Website |  + posts
Share This Article