ELOG yataka uchaguzi mkuu wa mwaka 2022 kukaguliwa

Martin Mwanje
1 Min Read

Kundi la Uangalizi wa Uchaguzi, ELOG sasa linataka uchaguzi mkuu wa mwaka 2022 kupigiwa darubini kwa mapana na marefu.  

ELOG inasema hatua hiyo itasaidia kutambua mapungufu makubwa yaliyopo kwenye mfumo wa uchaguzi katika hatua inayoweza kusaidia kuangazia mizozo inayotokana na matokeo ya uchaguzi.

Wanachama wa kundi hilo walitoa wito huo walipofika mbele ya Kamati ya Kitaifa ya Maridhiano inayoongozwa na kiongozi wa wengi katika bunge la Taifa Kimani Ichung’wah na kinara wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka.

Uangaziaji wa uchaguzi wa mwaka  2022 ni miongoni mwa masuala yanayotarajiwa kujadiliwa na kamati hiyo.

Baadhi ya makundi yaliyofika mbele ya kamati hiyo yamependekeza uchaguzi wa urais ufanywe siku tofauti na chaguzi zingine katika hatua ya kuboresha uwazi katika mchakato wa uchaguzi.

Muungano wa Azimio kwa upande wake unapendekeza kuchaguliwa kwa wanasiasa kuhudumu kama makamishna wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka, IEBC, pendekezo ambalo limepingwa vikali na utawala wa Kenya Kwanza.

Kulingana na Kenya Kwanza, hatua hiyo itaingilia uhuru wa IEBC.

Kadhalika Azimio imekuwa ikishinikiza kukaguliwa kwa uchaguzi wa mwaka 2022 ikidai ilishinda uchaguzi huo.

Hata hivyo, Kenya Kwanza imepuuzilia mbali shinikizo hizo ikisema hata Mahakama ya Upeo ilibaini kuwa iliibuka kidedea katika uchaguzi huo uliokuwa na ushindani mkubwa.

Share This Article