Ellen DeGeneres na Portia de Rossi wahamia Uingereza

Marion Bosire
1 Min Read

Ellen DeGeneres na Portia de Rossi wameondoka Marekani na kuhamia Uingereza baada ya Donald Trump kushinda kwenye uchaguzi mkuu.

Wanandoa hao wanaripotiwa kupata makazi mapya katika eneo la Cotswolds kusini magharibi mwa Uingereza umbali wa saa mbili kutoka London.

Nyumba hiyo inaaminika kununuliwa kabla ya uchaguzi na wakaamua kuhamia huko Trump aliposhinda.

Ellen ni mmoja kati ya watu maarufu nchini Marekani waliofadhili kampeni ya naibu rais Kamala Harris ambapo alimpa dola elfu 3,300.

Alimuunga mkono pia kupitia mitandao ya kijamii alipotangazwa kuchukua mahala pa Rais Joe Biden katika uwaniaji urais katika chama cha Democratic.

“Hakuna kitu kilicho na nguvu zaidi ya mwanamke ambaye wakati wake umefika. Nasubiri kwa hamu kuona Kamala Harris akiwa rais wetu.” aliandika Ellen wakati huo.

Ellen na Portia sasa wanapanga kuuza nyumba yao ya Montecito, California nchini Marekani ambako pia waliuza nyumba yao ya awali kwa dola milioni 96.

Watu wengi maarufu walitishia kuondoka Marekani kabla ya uchaguzi iwapo Trump angeshinda lakini Ellen ndiye wa kwanza kutekeleza hilo.

Wengine ni pamoja na Eva Longoria, America Ferrera, Laverne Cox, Cher na Sophie Turner.

Share This Article