Elias Kiptum Maindi amehukumiwa kifungo cha mwaka mmoja unusu gerezani kwa kosa la kupanga kuchafua sifa za wanariadha wa Kenya kupitia kwa sakata bandia za ulaji muku.
Mahakama ya uwanja wa ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyatta, imemhukumu Kiptum kupanga njama kutoa habari za uongo kwa wanahabari wa ugaibuni ili kuonyesha kuwa Kenya ina visa vingi vya utumiaji wa dawa za kutumua misuli.
Kiptum amepatikana na hatia ya makosa 13 na kuhukumiwa kifungo cha mwaka mmoja unusu kwa kila kosa hukumu ambayo itaenda sambamba.
Mshtakiwa wa pili kweny kesi hiyo ambaye ni mwanariadha mstaafu Paul Simbolei, alipatikana na kosa la kupanga njama ya kughushi,ili kuleta madhara kwa taifa na ameachiliwa huru baada ya koti kusema kuwa tayari amehudumu kwa muda zaidi ya kifungu alichostahili kupewa.
Kwenye uamuzi uliosomwa Jumanne na Hakimu Mkuu Njeri Thuku ,Kenya haijawahikuwa na visa vyovyote vya serikali vinavyohusiana na ulaji muku jinsi wawili hao walivyokuwa wakitaka kuashiria.
Jaji huyo ameongeza kuwa kesi hiyo ilinuia kuchafua sifa za Kenya endapo makala hiyo ingepeperushwa.
Hata hivyo Kiptum amepewa makataa ya wiki mbili kukata rufaa.
Mahakama hiyo hata hivyo ilikatalia mbali ombi la shirika la ulaji muku nchini ADAK kumhukumu Kiptum kifungo cha miaka mitatu gerezani katika kesi hiyo iliyoanza Juni mwaka 2021.