EFF: Vijana wa Gen Z waendelee kusimama kidete

Martin Mwanje
2 Min Read

Chama cha Economic Freedom Fighters (EFF) cha Afrika Kusini kimeelezea kuunga mkono maaandamano ya vijana wa Gen Z wanaoshinikiza kutekelezwa kwa mabadiliko nchini. 

EFF imewataka vijana hao kusimama imara hadi matakwa yao yote yaangaziwe na serikali. Ni msimamo unaokinzana na miito ya baadhi ya washikadau kama vile kanisa la ACK ambalo limewataka vijana hao kusitisha maandamano hayo ili kutoa fursa ya matakwa yao kushughulikiwa na serikali.

Isitoshe, chama hicho kinachoongozwa na Julius Malema kimewapongeza vijana wa Gen Z kwa kusimama kidete na kupinga Mswada wa Fedha 2024 ambao kinadai ulifadhiliwa na Benki ya Dunia na Shirika la Fedha Duniani, IMF.

Katika taarifa iliyotolewa leo Jumatatu, EFF kadhalika imelaani matumizi ya taasisi za kijasusi kuwakandamiza waandamanaji.

“…Tunalaani vikali matumizi ya taasisi za kijasusi kukandamiza maandamano haya ya haki, ambayo sasa yameguka na kuwa ya kumtaka Rais Ruto kujiuzulu,” ilisema taarifa ya chama hicho ambacho kimekuwa na hulka ya kuzungumzia maandamano hayo mara kwa mara.

“Mauaji ya kikatili ya waandamanaji vijana, kwa kutumia risasi hai na pia operesheni za kisiri zinazowalenga viongozi wa vijana hao ni ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu.”

Chama cha EFF pia kimepuuzilia mbali mpango wa kuunda serikali ya muungano inayouhusisha upande wa upinzani ili kuangazia matakwa ya vjana ikiutaja mpango huo kuwa unaokusudia kuufumba umma macho bila kuangazia masuala yaliyoibuliwa.

“Vijana wa Kenya wanapaswa kusimama imara hadi matakwa yao halali yatimizwe kikamilifu,” kiliongeza chama hicho kinachofahamika kwa kuwa na misimamo mikali nchini Afrika Kusini.

Matamshi ya chama hicho yanakuja wakati vijana wa Gen Z wametishia kufanya maandamano kwa siku nne mfululizo kuanzia kesho Jumanne.

Kutokana na hilo, baadhi ya shule za kutwa tayari zimewataka wanafunzi kusalia nyumbani hiyo kesho kwa hofu ya kutokea kwa vurugu kama ilivyoshuhudiwa siku zilizopita.

Rais William Ruto ameahidi kukabiliana vikali na yeyote mwenye nia ya kusababisha vurugu nchini na kuharibu mali ya wengine.

 

Website |  + posts
Share This Article