Edwin Kiplangat Bett na Diana Chepkorir ndio mabingwa wa mkondo wa sita na wa mwisho wa mbio za nyika za Kisii zilizoandaliwa leo katika shule ya upili ya Cardinol Otunga ,Mosocho.
Bett wa Kenya Police ameziparakasa mbio za kilomita kwa dakika 29 sekunde 55.8,akifuatwa na Asbel Kiprono wa North Rift kwa muda wa dakika 30 sekunde 5.6,huku Francis Kipkorir Langat akimaliza wa tatu kwa dakika 30 sekunde 10.6.
Diana Chepkorir kutoka KDF ameshinda mbio za kilomita 10 kwa dakika 33 sekunde 5.4,akifuatwa na Janeth Chepng’etich wa Nakuru kwa dakika 33 sekunde 32.8, naye Gladys Kwamboka wa Police akatwaa nafasi ya tatu kwa dakika 34 sekunde 11.8.
Emmanuel Lemiso alishinda mbio za Kilomita 8 wanaume chini ya umri wa miaka 20, kwa kutumia dakika 23 sekunde 56.4 ,akifuatwa na Emmanuel Yegon katika nafasi ya pili huku Ronald Ngetich akiridhia nafasi ya tatu.
Joyline Chepkemoi alishinda kilomita 6 wasichana wasiozidi umri wa miaka 20 akizitimka kwa dakika 19 sekunde 54.1,akifuatwa na Cynthia Chepkurui kwa dakiak 19 sekunde 54.2 wakati Diana Chepkemoi akichukua nafasi ya tatu.
Mashindano hayo sasa yatafuatwa na mbio za nyika baina ya kaunti Jumamosi ijayo na yale baina ya maeneo ya Januari 25 na hatimaye mashindano ya kitaifa ya mbio za Nyika Februari 25.