Mshindi wa nishani ya fedha ya dunia katika mita 10,000 Daniel Ebenyo Simiu na Viola Chepngeno, ndio mabingwa wa kilomita 10, katika msururu wa nne wa mbio za nyika nchini ulioandaliwa leo Bomet Airstrip kaunti ya Bomet.
Ebenyo alikata utepe kwa dakika 34 sekunde 25,29,akifuatwa na Edwin Edwin Bett wa kambi ya Keringet, aliyetumia dakika 32 sekunde 33.73, huku Peter Tuitoek akimaliza wa tatu kwa kutumia dakika 32 sekunde 54.05.
Ebenyo amesema ametumia mashindano ya leo kujipima kwa msimu ujao baada ya kutatizwa na msururu wa majeraha .
Katika mbio za kilomita 10 wanawake , Viola Chepngeno kutoka kambi ya wanariadha ya Keringet , ameibuka mshindi alimpotimka kwa dakika 37 sekunde 6.68,akifuatwa na Sandrafelis Chebet kwa dakika 37 sekunde 30.15, huku Joyline Cherotich akiridhia nafasi ya tatu kwa dakika 37 sekunde 40.25.
Florence Chepkoech alishinda kilomita sita wasichana wasiozidi umri wa miaka 20 kwa dakika 21 sekunde 48.8,akifuatwa na Alice Chemtai na Cynhtia Chepkurui katika nafasi za pili na tatu mtawalia.
Emmanuel Lemiso wa Nakuru ameshinda kilomita 8 wavulana chini ya umri wa miaka 20 akiziparakasa kwa dakika 26 sekunde 17.26.
Clinton Kimutai na Brian Kiptoo walimaliza katika nafasi za pili na tatu mtawalia.
Reynold Cheruiyot na Nelly Chepchirir walishinda kilomita 2 mzunguko .