Maafisa wa tume ya kukabiliana na ufisadi hapa nchini EACC, wamewakamata washukiwa wawili kwa madai ya kuwalaghai maafisa wa kuu serikalini.
Francis Onyango na Abigail Janai, walionuia kumlaghai Mkurugenzi mmoja Mkuu wa shirika moja la serikali shilingi milioni mbili, kwa kisingizio wangeweza kumsaidia kuondoa kesi inayomkabili mahakamani.
Kupitia mtandao wa X leo Jumatano, EACC ilisema baada ya kupokea habari kuhusu wawili hao, ilianzisha operesheni ya kuwasaka, na kuwatia nguvuni katika kituo kimoja cha burudani, baada ya kupokea shilingi milioni 1.7, ikiwa sehemu ya malipo ya shilingi milioni mbili walizokuwa wameitisha.
Kulingana na tume hiyo, wawili hao walihojiwa katika kituo cha polisi kilicho katika makao makuu ya EACC, kabla ya kuzuiliwa katika kituo cha polisi cha Kilimani.
Tume hiyo ilisema wawili hao ni sehemu ya kundi la watu wanaojisingizia kuwa maafisa wa umma, ambao huwashtaki maafisa wakuu wa serikali na kisha kuwaitisha hongo ili waondoe kesi hizo mahakamani.