Itachukua muda mrefu kufanikisha vita dhidi ya ufisadi humu nchini iwapo vita hivyo vitaachiwa Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) pekee.
Wakizungumza mjini Machakos wakati wa ufunguzi wa warsha ya siku moja ya maafisa wakaguzi wa bajeti za wafanyakazi wa serikali, maafisa kutoka EACC wameeleza umuhimu wa ushirikiano baina ya washikadau mbalimbali kufanikisha vita dhidi ya ufisadi.
Wamesema ingawa tume hiyo imejizatiti katika vita dhidi ya ufisadi, kufikia sasa bado zipo changamoto si haba za ushirikiano na mara kwa mara kukwamisha juhudi za EACC kukabiliana na ufisadi nchini.
Kulingana na Jocye Ominya kutoka Taasisi ya Wakaguzi wa Ndani (IIA), zipo changamoto hususan utoaji wa habari kuhusu uwezekano wa visa vya ufisadi katika mashirika ya serikali na ulinzi wa wanaofichua ufisadi.
Kikao hicho cha siku moja kimewaleta pamoja washikadau kutoka mashirika mbalimbalj ya serikali kutathimini njia mwafaka za kuzuia ufisadi serikalini.