Baadhi ya wanawake katika kaunti ya Mombasa, wametoa wito kwa tume ya maadili na vita dhidi ya ufisadi (EACC), Kumchunguza mwakilishi wa kike wa kaunti hiyo Zamzam Mohamed, kwa madai ya utovu wa maadili na kiburi.
Wanawake hao wametisha kuanza mchakato wa kukusanya saini kwa lengo la kumuondoa mamlakani kuambatana na katibu na sheria za uchaguzi.
Wanawake hao walisababisha msongamano wa magari walipoandamana kutoka mzunguko wa barabara wa Makupa hadi ofisi ya mwakilishi huyo wa kike iliyoko Tudor, katika eneo bunge la Mvita.
Esther John mkazi wa mmoja wa Changamwe, alidai kuwa mwakilishi huyo wa kike hawaheshimu viongozi wengine waliochaguliwa, anawafuta kazi kiholela wafanyakazi katika ofisi yake na kutoa msaada wa masomo kwa watu wasiokuwa wakazi wa kaunti ya Mombasa.
Aidha, John alimshtumu mume wa mbunge huyo wa kaunti kwa kuongoza afisi hiyo.
“Tulimchagua mwakilishi mwanamke na wala sio naibu mwakilishi mwanamke. Afisi hiyo inaongozwa na mume wake. Anaongoza mikutano katika afisi hiyo,” alisema John.