EACC yamkamata afisa wa polisi kwa kula mlungula

Tom Mathinji
1 Min Read

Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) jana Alhamisi ilimtia nguvuni afisa wa polisi anayehudumu katika kituo cha polisi cha Mumias kaunti ya Kakamega, kwa kuitisha na kupokea hongo.

Kulingana na taarifa, Joshua Ouma Odour alikamatwa kwa kupokea hongo ili kufanikisha kuachiliwa kwa gari ambalo lilikuwa likizuiliwa katika kituo hicho cha polisi.

Gari hilo lilizuiliwa kwa madai kuwa nambari zake za usajili zilikuwa zimefutika.

Afisa huyo alipelekwa katika afisi za tume ya  EACC zilizoko  kaunti ya Bungoma, kabla ya kuzuiliwa katika kituo cha polisi cha Bungoma.

Tume hiyo ilipokea malalamishi jana Alhamisi na kuanzisha uchunguzi uliosababisha kutiwa nguvuni kwa afisa huyo  alipokuwa akipokea hongo.

Aidha EACC imewahimiza watumishi wa umma kutumia nyadhifa zao kuwahudumia wananchi kwa uadilifu.

“Sio tu uhalifu lakini pia ni utovu wa maadili kwa afisa wa umma kuitisha na kupokea hongo kwa sababu yoyote ile,” ilisema EACC.

TAGGED:
Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *