EACC yamkamata afisa wa mapato wa Kilifi kwa tuhuma za rushwa

Martin Mwanje
1 Min Read
Sylvia Dhahabu Karisa anayetuhumiwa kwa makosa ya rushwa

Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) imemkamata afisa wa mapato wa serikali ya Kilifi kwa tuhuma za hongo na utumiaji mbaya wa afisi yake.  

Mshukiwa, Sylvia Dhahabu Karisa, Mkaguzi wa Majengo anayefanya kazi katika kitengo cha Uidhinishaji cha Manispaa ya  Watamu, anadaiwa kuitisha shilingi 435,000 kutoka kwa mlalamikaji ili kumsaidia kupata kibali cha ujenzi. 

Kulingana na mlalamikaji, maafisa wa mapato wa kaunti walitembelea eneo lake la ujenzi katika eneo la Timboni huko Watamu na kuitisha shilingi 73,000 za ujenzi wa ukuta na shilingi 362,000 za miundominu mingine. Fedha hizo zinasemekana kuongezwa kimakusudi kwa manufaa ya kibinafsi. 

Baada ya kupokea taarifa kutoka kwa mlalamikaji Machi 25, 2026, EACC ilifanya uchunguzi wa awali uliothibitisha kuwa hongo ya shilingi 400,000 ilikuwa imeitishwa.

Kisha operesheni ilifanywa jana Alhamisi na kusababisha kukamatwa kwa mshukiwa katika afisi za manispaa za Watamu. 

Mshukiwa alipelekwa katika afisi za EACC za kanda ya Pwani mjini Malindi kuandikisha taarifa na kisha katika kituo cha polisi cha Malindi.

Aliachiliwa kwa dhamana ya shilingi 20,000 huku uchunguzi ukiendelea.

Share This Article