EACC yalalamikia mabadiliko kwenye mswada wa mkinzano wa maslahi

Marion Bosire
2 Min Read

Tume ya maadili na kupambana na ufisadi EACC imeonyesha kutoridhika na hatua ya bunge la Seneti ya kufanya mabadiliko kwenye mswada wa mkinzano wa maslahi wa mwaka 2023.

EACC inalalama kwamba bunge hilo limetoa vipengee muhimu na kuongeza vingine ambavyo vinahujumu vita dhidi ya ufisadi.

Akizungumza huko Tharaka Nithi, hatibu wa EACC Eric Ngumbi alisema mswada huo ukitiwa saini na Rais utakubalia maafisa wa serikali kupata zabuni za serikali huku wakijikinga pamoja na familia zao dhidi ushuru na kulemaza juhudi za EACC za kukabiliana na ufisadi.

Tume hiyo inasema pia kwamba mswada huo ulibuniwa na baraza la mawaziri kama mbinu ya kupambana na ufisadi na kukabidhiwa viongozi wa wengi katika mabunge ya seneti na kitaifa.

Katika mabadiliko yaliyofanywa, maseneta wanadaiwa kuondoa vipengee 20 na kurekebisha vingine zaidi ya 15.

Wadau katika EACC wanaomba wabunge wa bunge la taifa kutokubali mabadiliko yaliyofanyiwa mswada huo na bunge la seneti na badala yake kuondoa mabadiliko hayo na kuujadili upya.

EACC inatilia shaka pia mswada wa marekebisho ya sheria ya kupambana na ufisadi na makosa ya kiuchumi wa mwaka 2023 uliowasilishwa na mbunge wa Mbeere Kaskazini Geoffrey Ruku unaopendekeza kuondolewa kwa sehemu ya 45(2).

Kipengee hicho kinalenga kuharamisha vipengele fulani vya manunuzi, mauzo ya mali ya serikali, kutuma maombi ya kupata zabuni, usimamizi wa fedha na matumizi.

Mswada wa Ruku unalenga kuondoa makosa mawili makuu ya ufisadi yaliyoainishwa kwenye sheria hiyo kwa lengo la kulinda pesa za umma dhidi ya kufujwa na maafisa wa serikali wanaohusika katika usimamizi wake.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *