EACC yaanza kuifanyia NHIF ukaguzi wa mifumo, nia ni kuziba mianya ya ufisadi

Martin Mwanje
1 Min Read

Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi, EACC leo Alhamisi imeanza kufanya ukaguzi wa mifumo, sera na shughuli za Hazina ya Kitaifa ya Bima ya Afya, NHIF. 

Katika taarifa, EACC inasema dhamira ya ukaguzi huo ni kutambua na kuziba mianya na mapungufu yanayosababisha kukithiri kwa ufisadi katika hazina hiyo.

Matokeo ya utafiti huo yatatoa mwongozo wa hatua mbalimbali za mabadiliko yatakayofanyiwa hazina hiyo ikiwa ni pamoja na kuangazia mapungufu ya uwajibikaji katika usimamizi wa rasilimali za umma zinazosimamiwa na NHIF.

“Zoezi la ukaguzi, litakalozinduliwa katika chumba cha mikutano cha NHIF, ni hatua ya kuzuia ufisadi, ambayo kwa namna yoyote haiathiri uchunguzi unaoendelea katika hazina hiyo,” inasema taarifa ya EACC.

Tume hiyo inaongeza kuwa imepewa mamlaka ya kufanya ukaguzi kama huo wa mifumo katika taasisi za umma kwa hiari yake au kutokana na mwaliko kutoka kwa taasisi husika.

Ukaguzi huo unakuja wakati ambapo NHIF kwa sasa inafanyiwa uchunguzi na kamati ya afya ya bunge la taifa kuhusiana na madai ya kukithiri kwa ufisadi katika hazina hiyo.

Share This Article