EACC kutwaa mali ya aliyekuwa mfanyakazi wa serikali ya kaunti ya Machakos

Marion Bosire
2 Min Read

Tume ya maadili na kupambana na ufisadi nchini EACC imepata maagizo kutoka kwa mahakama kuu ya kutwaa mali ya thamani ya zaidi ya shilingi milioni 91, ya Urbanus Wambua Musyoka.

Wambua ambaye aliwahi kuhudumu kama mwanachama wa kamati kuu ya kaunti ya Machakos kati ya Januari 2014 and Julai 2021, anasemekana kupata mali hiyo kupitia ufisadi, mkinzano wa maslahi na ulaghai.

Mali hiyo inajumuisha jengo la makazi la thamani ya shilingi milioni 80,251,815 na pesa kwenye akaunti za benki za Co-operative Bank na Equity Bank.

EACC kupitia msemaji wake Eric Ngumbi imeridhika na uamuzi wa jaji P.J. Otieno wa mahakama ya Milimani aliotoa Oktoba 28, 2024.

Ngumbi amefichua kwamba kesi hiyo ni moja kati ya mbili za kurejesha mali ya umma ya thamani ya shilingi milioni 548,250,106 kutoka kwa Musyoka zinazofuatiliwa na EACC.

Kesi ya pili inaendelea katika mahakama kuu na inahusisha shilingi milioni 457,047,214.80 ambazo Musyoka alipokea visivyo kupitia malipo ya zabuni hewa kwa kampuni zinazomilikiwa na mke wake, kakake na marafiki zake.

EACC ilielekea mahakamani baada ya Musyoka, aliyekuwa akisimamia masuala ya kilimo, usalama wa chakula na ustawi wa vyama vya ushirika na mwenyekiti wa kamati ya utoaji zabuni kukosa kuelezea kuhusu kutolingana kwa mali yake na mshahara aliokuwa akilipwa.

Uchunguzi wa EACC ulibaini kwamba Musyoka alifaidi visivyo kutokana na malipo ya zabuni zilizotolewa kwa kampuni zinazomilikiwa na mkewe Fiona Muthoki Mutisya, nduguye Antony Mbindyo Musyoka na marafizki zake.

Kampuni hizo zilipokea jumla ya shilingi milioni 457,047,214.80.

EACC iliamua kumshtaki Musyoka na wenzake ambao walikamatwa Novemba, 2023 na kufikishwa katika mahakama ya kupambana na ufisadi ya Machakos ambapo walikanusha mashtaka.

Website |  + posts
Share This Article