Uunganishaji wa kidijitali umetajwa kuwa kichocheo kikuu katika ustawi wa biashara, uwekezaji, utoaji huduma na kufanikisha ushiriki wa raia katika kanda ya Afrika Mashariki.
Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashriki anayehusika na maswala ya Miundombinu, uzalishaji, na sekta za kijamii na kisiasa Andrea Aguer Ariik Malueth, alisema hayo siku ya Alhamisi kwenye mkutano wa viongozi wa Mashirika ya Mawasiliano Afrika Mashariki.
Malueth alisema mapendekezo kwenye mkutano huo yanalenga kutoa suluhu ambazo zitaimarisha jinsi raia, wafanyabiashara na wasafiri wanavyotangamana katika maisha yao ya kila siku kwenye kanda hiyo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Halmashauri ya Mawasiliano ya Tanzania Mhandisi Peter Mwasalyanda, alielezea kujitolea kwa Tanzania kufanikisha utangamano wa kidijitali na kuwezesha ushindani katika sekta ya mawasiliano.
Kwenye hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na John Wallace Daffa ambaye ni Mkurugenzi wa utoaji leseni na uzingatiaji sheria, Mwasalyanda alidokeza kuwa mageuzi yanayoendelea kwenye utumizi wa mtandao wa simu wa kanda, yamesababisha kupungua kwa gharama ya utumizi wa simu katika kanda ya Afrika Mashariki.
“Sasa tunashuhudia manufaa wakati tunaposafiri katika kanda hii. Utumiaji wa mtandao wa simu sio kama starehe. Swala hili limewiainishwa katika ruwaza ya EAC ya usafiri huru wa watu na bidhaa, utoaji huduma na kupunguza gharama ya kufanya biashara,” alisema Mwasalyanda,
Huku akimwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Mawasiliano ya Uganda Nyombi Thembo, Mkurugenzi wa Uhandisi na Mawasiliano ya Miundombinu Alfred Joseph Bogere, alisisitiza umuhimu wa kuhakikisha hakuna mwananchi anatengwa wakati huu wa enzi ya dijitali.
“Tunatambua kuwa upatikanaji wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICT), sasa ni muhimu sawia na elimu, huduma za afya, biashara, uongozi, ajira na ushiriki wa kijamii, na umekuwa nguzo kuu katika utangamano wa kikanda,” alisema Mhandisi Bogere.
Mkutano huo ulipigia kurunzi maswala kadhaa ikiwa ni pamoja na mifumo ya uwekaji bei, ulinzi wa wateja, uzingatiaji sheria, mbinu za utatuzi wa mizozo, na ushirikishi wa operesheni zinazohitajika kutekeleza mtandao wa simu wa kanda uliowiainishwa.
Mkutano huo ulioandaliwa Jijini Dar es Salaam, Tanzania siku ya Alhamisi, ulilenga kuhakikisha upatikanaji wa mtandao nafuu wa simu ili kuimarisha uunganishaji, biashra na utangamano wa raia wa kanda ya Afrika Mashariki.
Waliohudhuria mkutano huo ni pamoja na wataalam wa kiufundi, mashirika ya mawasiliano ya kanda hiyo, halmashauri za udhibiti na washirika wa maendeleo.
Halmashauri za kitaifa za kudhibiti mawasiliano hutekeleza wajibu muhimu katika utekelezaji shwari wa mkakati wa mtandao wa simu kwa kuhakikisha huduma za simu za kanda zinasalia kuwa za gharama nafuu, za kutegemewa na zinazokidhi mahitaji ya wateja katika Jamii ya Afrika Mashariki.