Duan Davis ashtakiwa kwa mauaji ya Tupac Shakur

Marion Bosire
2 Min Read
Tupac Shakur na Keffe D

Duane Davis maarufu kama Keffe D wa umri wa miaka 60, alishtakiwa na maafisa wa polisi katika mahakama ya Nevada kwa mauaji ya mwanamuziki Tupac Shakur yaliyotokea mwaka 1996.

Shakur mzaliwa wa New York, ambaye alikuwa mwanamuziki wa mtindo wa hip hop alipigwa risasi mara nne jijini Las Vegas akiwa na umri wa miaka 25.

Mshambuliaji wake alikuwa kwenye gari ambalo lilipita gari lake.

Kulingana na maafisa wa polisi Keffe D alipanga mauaji ya Shakur baada ya mpwa wake aliyekuwa akiitwa Orlando Anderson kuzozana na Shakur katika kituo kimoja cha michezo ya kamari muda mfupi kabla ya kisa hicho kutokea Septemba 7,1996.

Anderson ambaye anaaminika kuwa mwanachama wa kundi haramu lililokuwa likiongozwa na Davis aliaga dunia Mei 29, 1998 baada ya ufyatulianaji risasi na wanachama wengine wawili wa kundi haramu.

Davis alikamatwa karibu na makazi yake ya Las Vegas asubuhi ya Ijumaa Septemba 29, 2023.

Afisa wa polisi aliyestaafu kwa jina Greg Kading, ambaye alikuwa akichunguza kesi ya mauaji ya Tupac kwa miaka mingi aliambia wanahabari kwamba kukamatwa kwa Davis sio jambo la kushtua kwake.

Kulingana Kading, wahusika wengine wote wa kisa hicho cha mauaji wameshaaga dunia na Davis pekee ndiye amesalia.

Davis amehojiwa na wanahabari mara kadhaa ambapo anasikika akikiri kwamba alikuwa kwenye gari ambayo mshambuliaji wa Tupac alikuwa wakati wa kisa hicho.

Shakur alipelekwa hospitalini ambako alilazwa na akaaga siku sita baadaye.

Share This Article