Waziri wa mazingira Aden Duale, amesema wakenya tayari wamepanda miche Milioni 481 ya miti tangu mwezi Januari mwaka huu, kama sehemu ya juhudi za kukabiliana na athari za Mabadiliko ya Tabia Nchi.
Akiongea leo Alhamisi katika bustani ya Arboretum Jijini Nairobi wakati wa maadhimisho ya siku kuu ya Mazingira, Waziri Duale aliwapongeza wananchi kwa kushiriki kwenye kampeini ya serikali ya kupanda miti bilioni 15 kufikia mwaka 2032.
Aliangazia athari za Mabadiliko ya Tabia Nchi humu nchini, na akawahimiza wakenya wote wafanye juhudi za kupanda miti zaidi ili kuhakikisha mazingira bora.
Duale pia alizungumzia suala la uchafuzi wa mto Nairobi, akisema serikali imeahidi kuunadhifisha katika muda wa miezi 18 ijayo.
Ili kuepusha uchafuzi wa mazingira, waziri alisema wiki ijayo atachapisha kwenye gazeti rasmi la serikali nembo za rangi za taka kutoka katika nyumba za watu za kutofautisha taka zinazoweza kustawishwa upya kwa matumizi na zile zinazopasa kutupwa.
Serikali ilibadili jina la siku kuu ya Utamaduni day kuwa mazingira Day mwezi Aprili mwaka huu ili kuwahimiza wakenya kushiriki kikamilifu katika juhudi za uhifadhi wa mazingira.