Aden Duale, ambaye alihudumu kama waziri wa ulinzi katika baraza lililovunjwa na Rais William Ruto kabla ya kurejeshwa kwenye wadhifa huo huo amemshukuru Rais kwa kumhamishia wizara nyingine.
Kwenye ujumbe aliochapisha kwenye akaunti yake iliyothibitishwa ya mtandao wa X Duale aliandika, “Ninamshukuru Rais William Ruto kwa kunihamisha kutoka wizara ya ulinzi hadi wizara ya mazingira, mabadiliko ya tabianchi na misitu.”
Katika ujumbe wake Duale aliahidi kuendelea kutoa huduma katika wadhifa huo mpya ambapo amesema ataangazia zaidi usimamizi endelevu wa mazingira, kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kuhakikisha kurejeshwa kwa misitu nchini.
Alinukuu kufungu cha kitabu kitakatifu cha dini ya kiisilamu Quran 2:216 kisemacho, “Na huenda ikawa kwamba hupendi kilicho kizuri kwako na unapenda kilicho kibaya kwako.”
Katika orodha ya mawaziri wa kwanza 11 aliowateua Rais, Duale alirejeshwa kwenye wizara ya Ulinzi huku mwenzake Soipan Tuya akirejeshwa kwenye wizara ya mazingira, mabadiliko ya tabianchi na misitu.
Tuya sasa ameteuliwa kwa wadhifa wa waziri wa ulinzi ambao ulishikiliwa awali na Duale.
Mabadiliko haya yaliwasilishwa na Rais Ruto kwa spika wa bunge la taifa Moses Wetangula kwani bunge linajiandaa kusaili walioteuliwa kabla ya kuwasilisha ripoti kwa Rais kwa uteuzi kamili.
Spika Wetangula alikuwa anawajuza wabunge kuhusu kuwasilishwa bungeni kwa majina 11 ya mawaziri kwa usaili alipotangaza mabadiliko hayo.
Majina hayo yamewasilishwa kwa kamati ya bunge kuhusu uteuzi ambayo inatarajiwa kuwasaili na kuwasilisha ripoti katika muda wa siku 28.