Drake atangaza mapumziko kutoka muziki ili kuangazia afya yake

Marion Bosire
2 Min Read

Punde tu baada ya kutoa albamu yake mpya kwa jina “For All The Dogs” mwanamuziki Drake ametangaza kwamba anachukua mapumuziko ya muda kutoka kwa kazi ya muziki ili kuangazia afya yake.

Akizungumza kwenye mahojiano, mwanamuziki huyo ambaye jina lake halisi ni Aubrey Drake Graham, hakutoa maelezo ya undani kuhusu anachougua lakini alisema tu kwamba kwanza anahitaji kuangazia afya yake na kwamba hivi karibuni ataelezea mengi zaidi.

Baadaye kwenye mahojiano hayo, Drake wa umri wa miaka 36 sasa na ambaye ni wa asili ya Canada alisema kwamba amekuwa na matatizo ya tumbo kwa muda sasa na ni lazima ashughulikie tatizo hilo kwani anapendelea watu wakiwa na afya njema.

Drake amekuwa akizunguka na mwanamuziki mwenza kwa jina “21 Savage” kwenye ziara yao ya kikazi nchini Marekani ambayo waliipa jina la “It’s All a Blur” tangu Julai. Ziara hiyo ya matamasha 56 katika sehemu mbali mbali Marekani kaskazini itafikia kikomo mwisho wa mwezi huu wa Oktoba.

Naye kama mwanamuziki binafsi amekuwa na kazi nyingi katika muda wa miaka michache iliyopita ambapo mwaka jana pekee alitoa albamu mbili, ya kwake iitwayo “Honestly, Nevermind” na nyingine waliyoshirikiana na 21 Savage iitwayo “Her Loss”.

For All The Dogs ndiyo albamu yake ya nane na ina nyimbo 23.

Share This Article