Dozi 10,700 za Modified Vaccinia Ankara-Bavarian Nordic (MVA-BN) zimewasili ili kusaidia kukabiliama na mlipuko wa ugonjwa wa Mpox humu nchini.
Wizara ya Afya inasema chanjo hizo zilipokelewa nchini kutokana na ushirikiano kati ya serikali ya Kenya na Kituo cha Kudhibiti Ugonjwa barani Afrika (Africa CDC), Shirika la Afya Duniani (WHO), UNICEF, Gavi na Vaccine Alliance.
“Kuwasili kwa chanjo hizo ni mwanzo wa hatua kubwa ya mwitikio wa taifa kusimamisha mtungo wa usambazaji, na kukomesha msambao zaidi wa ugonjwa wa Mpocx katika jamii,” alisema Waziri wa Afya Aden Duale katika taarifa.
“Chanjo ni moja ya hatua bora zaidi za kushughulikia afya ya umma, zikiokoa mamilioni ya maisha kila mwaka, na kutumiwa kote duniani kuhamasisha afya ya umma, kuzuia na kudhiti milipuko, na kwa kufanya hivyo kupunguza maafa kutokana na magonjwa yanayoweza kuzuiwa na chanjo.”
Tangu kutangazwa kwa mlipuko wa ugonjwa wa Mpox Julai 31, 2024, jumla ya visa 67 ya ugonjwa huo vimethibitishwa katika kaunti 13 kote nchini.
Kaunti zilizoathiriwa na ugonjwa huo ni pamoja na Busia iliyoripoti visa 22, Mombasa (12), Nakuru (10), Makueni (6) na Bungoma (3).
Kaunti zingine zilizoathiriwa ni Nairobi (3), Kajiado (2), Taita Taveta (2), Kericho (2), Kilifi (2), Kiambu (1), Uasin Gishu (1) na Migori (1).
Mtu mmoja amefariki kutokana na ugonjwa huo hadi kufikia sasa.