Dorcas Rigathi: Msiwatenge waraibu wa mihadarati

Tom Mathinji
2 Min Read

Mke wa naibu Rais mchungaji Dorcas Rigathi, ametoa changamoto kwa wazazi walio na watoto ambao ni waraibu wa mihadarati, kuwakumbatia ili kuwasaidia kuacha utumizi wa dawa za kulevya.

Mchungaji Dorcas alisema watoto hao wanapaswa kuonyeshwa upendo na familia zao ili kufanikisha uponyaji wao.

Kulingana na mke huyo wa naibu wa Rais, kuwaonyesha vijana hao unyanyapaa na kuwatenga, kutahujumu safari yao ya kupiga kumbo utumizi wa mihadarati.

“Uraibu wa mihadarati na pombe ni sawa na ugonjwa. Huwezi washutumu watu wagonjwa, kile unachohitaji ni kuwaelewa na kuwasaidia kukabiliana na utumizi wa dawa za kulevya,” alisema mchungaji Dorcas.

Aidha alidokeza kuwa afisi yake inahakikisha waraibu wa mihadarati wanafanyiwa urekebishaji tabia katika vituo vya afya.

Aliyasema hayo Jumapili katika kaunti ya Kiambu, wakati wa mechi kati ya Jubilee Christian Church team na Heroes, mashindano ambayo yaliwaleta pamoja waraibu wa mihadarati ambao wamerekebishwa tabia kupitia mafunzo ya kiufundi na ushauri nasaha.

Akizungumza katika hafla hiyo, naibu wa kamishna kaunti ya Kiambu Titus Macharia, alisema eneo hilo limefanikiwa katika vita dhidi ya pombe haramu kutokana na juhudi za pamoja kati ya serikali na wananchi.

“Katika kaunti ya Kiambu tumepunguza utumizi wa pombe haramu kwa kiwango kikubwa,” alisema Macharia.

Naibu Rais Rigathi Gachagua amekuwa mstari wa mbele katika vita dhidi ya pombe haramu katika eneo la mlima Kenya.

Website |  + posts
Share This Article