Don Lemon asema masharti ya ulezi wa Wendy Williams ni makali mno

Hisia za Lemon zinatokana na mazungumzo yake ya hivi maajuzi na Wendy na zinawiana na uamuzi wa hivi karibuni zaidi wa jaji kuhusu mustakabali wake.

Marion Bosire
2 Min Read

Mtangazaji wa runinga nchini Marekani Don Lemon amesema kwamba masharti ya ulezi wa Wendy Williams ni makali mno na anafaa kuruhusiwa kuwa na watu wa familia yake.

Hisia za Lemon zinatokana na mazungumzo yake ya hivi maajuzi na Wendy na zinawiana na uamuzi wa hivi karibuni zaidi wa jaji kuhusu mustakabali wake.

Jaji anayeshughulikia suala la usimamizi na ulezi wa mtangazaji huyo wa runinga alimpa Wendy ruhusa ya kwenda Florida Kusini kuona babake na kusherehekea siku yake ya kuzaliwa anapotimiza umri wa miaka 94.

Uamuzi huo wa jaji unachukuliwa kuwa hatua muhimu katika mapambano ya Wendy ya kutafuta kuachiliwa kabisa kutoka kwa makazi ya kusaidiwa huko New York.

Wendy anarejelea nyumba yake ya chumba kimoja kwenye makazi hayo kuwa jela ya kifahari akisema huwa hapati fursa ya kutoka nje kupumua hewa safi, haruhusiwi kutumia mtandao na haruhusiwi kuwa na wageni.

Don, ambaye alimhoji Wendy wiki kadhaa zilizopita anasema hajaweza kuzungumza naye tena lakini anawasiliana na watu wa familia yake na anamtakia mema.

Anaomba apate uhuru kikamilifu au apatiwe huduma za kiafya.

Wendy alipatikana kuwa na ugonjwa wa akili uitwao dementia na ataandamana na mlinzi aliyeidhinishwa na mahakama atakapokwenda kumwona babake na atakaa huko kwa siku mbili tu kisha arejee New York.

Jaji amezuia Wendy kuwasiliana na wanahabari baada yake kufanya mahojiano na Don, Charlamagne Tha God na TMZ.

TMZ inapanga kuzindua maudhui yake kwa jina “Saving Wendy” Februari 12, 2025 kwenye jukwaa la Tubi.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *