Dogo Janja asherehekea siku yake ya kuzaliwa kwa njia ya kipekee

Marion Bosire
1 Min Read

Mwanamuziki wa Tanzania Dogo Janja jana Septemba 15, 2024 aliamua kusherehekea siku yake ya kuzaliwa kwa njia ya kipekee.

Nyota huyo wa muziki wa Bongo Fleva alizuru gereza kuu la Kisongo jijini Arusha ambapo alihusiana na wafungwa na kuwapa msaada wa vitu mbali mbali.

Dogo ambaye pia alikuwa anasherehekea miezi kumi tangu mwanawe azaliwe, aliwapelekea wafungwa hao viyu mbali mbali kama misala, champali, vifaa vya usafi kama miswaki pamoja na chakula.

“Kama unavyoelewa leo ni kumbukizi ya siku yangu ya kuzaliwa na mtoto wangu anajaza miezi kumi, hii ni sehemu ambayo mtu yeyote anaweza kuja, nimebeba vitu vingi sana ila vitu vya thamani kwangu nilivyovibebea ni hii miswala ya kuswalia, Biblia na Misaafu.” alisema Dogo.

Alisema ametimiza umri ambao ni ndoto ya kila Kijana na anashukuru Mungu kwa uhai anapoiunga mkono serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan.

Dogo Janja alitoa pia mchango wa kitambaa cha kuwashonea wafungwa sare za gerezani huku akihimiza wananchi wenzake kuendelea kuwaonyesha mapenzi wafungwa kwani wanahitaji faraja.

Share This Article