Mamlaka ya Afya ya Jamii (SHA) ina Afisa Mkuu Mtendaji mpya.
Uteuzi wa Dkt. Mercy Mwangangi kwenye wadhifa huo umetangazwa na Waziri wa Afya Aden Duale.
“Uteuzi wake unafuatia kuhitimishwa kwa mchakato wa usaili wenye ushindani ambao ulishuhudia jumla ya watu 92 wakituma maombi. Kati ya watu hao, 12 waliorodheshwa na kuhojiwa,” alisema Duale kwenye taarifa.
Dkt. Mwangangi kwa sasa anahudumu kama Mkurugenzi Mwandamizi wa Uimarishaji wa Mifumo ya Afya katika shirika la AMREF Health Africa.
Daktari huyo alipata kufahamika mno wakati alipohudumu kama Katibu Mkuu (CAS) wa Wizara ya Afya wakati wa utawala wa Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta.
Inatazamiwa kuwa atatumia tajiriba yake ya zaidi ya miaka 15 katika upatikanaji wa afya kwa wote (UHC) kulainisha utendakazi wa SHA ambayo imekubwa na changamoto za kila aina tangu kuzinduliwa kwake mwaka jana.
Anateuliwa katika widhifa huo na Waziri Duale ambaye siku chache zilizopita alipewa jukumu la kuongoza Wizara ya Afya baada ya kuhamishwa kutoka ile ya Mazingizra.
Wakati wa mkutano na maafisa wa Chama cha Madaktari nchini, KMPDU jana Alhamisi, Duale aliahidi kushirikiana na wahudumu wa afya kuboresha huduma za matibabu nchini wakati pia akihakikisha maslahi yao yanalindwa.