Serikali inatekeleza juhudi za kuboresha miundombinu katika magereza yote kote nchini. Hayo ni kwa mujibu wa Katibu wa Idara ya Magereza Dkt. Salome Beacco.
Kulingana na Dkt. Beacco, hatua hiyo itaimarisha utoaji huduma na mazingira ya wafungwa.
Akizungumza katika kaunti ya Bungoma baada ya kuzuru magereza ya wanaume na ya wanawake, Dkt. Beacco alidokeza kuwa miongoni mwa mapendekezo ya kuboresha magereza nchini ni pamoja na kuongeza idadi ya vitanda ili kuhakikisha maisha yenye heshima miongoni mwa wafungwa.
Katibu huyo alisema kuwa wafanyakazi katika makao makuu ya idara hiyo, watafanya ziara za kila mara katika afisi za mashinani kukadiria hali halisi ili kufanikisha mipango ya shughuli katika idara hiyo.
“Kama maafisa wakuu, hatutakaa afisini tu, tutatembea kuwasikiliza na kujadiliana moja kwa moja na maafisa walio mashinani,” alisema Dkt. Beacco.
Aliwapongeza maafisa wa magereza katika kaunti ya Bungoma kwa kutekeleza upanzi wa miti kwa wingi katika taasisi hizo, kuambatana na agizo la Rais la upanzi wa miti bilioni 15 kufikia mwaka 2032.