Diva na Niffer waandika taarifa za kuomba msamaha

Marion Bosire
1 Min Read
Niffer, mfanyabiashara Tanzania

Mtangazaji wa Wasafi Fm Diva Malinzi na mfanyabiashara Niffer wameandika jumbe za kuomba msamaha wakiwa katika kituo cha polisi.

Haya yanajiri siku moja tu baada ya wawili hao kukamatwa kwa makosa ya kuchangisha pesa kwa umma bila idhini inayostahili.

Wawili hao wameomba wachiliwe ili waendelee na shughuli zao za kawaida ikitizamiwa kwamba makosa yao yanaweza kuvutia kifungo cha hadi mwaka mmoja gerezani.

“Mimi Diva Giselle Malinzi naomba radhi kwa watanzania na serikali kwa jumla kwa kosa la kuchangisha fedha nje ya utaratibu.” aliandika mtangazaji huyo akisema alifanya mchango huo bila kufahamu taratibu ila sasa anafahamu.

Niffer naye alikiri kwamba sasa amejifunza kutokana na tukio hilo na wote wawili wameahidi kuwa mabalozi wa wazuru wa kuchangisha hela panapotokea dharura ila hawaombei dharura.

Wawili hao walitumia ufuasi wao mkubwa katika mitandao ya kijamii kuchangisha fedha wakati ajali ya kuporomoka kwa jengo la kibiashara ilitokea Kariakoo jijini Dar es Salaam Jumamosi.

Viongozi walikemea hatua hiyo huku mkuu wa mkoa wa Dar es salaam Albert Chalamila akitoa onyo kali na waziri mkuu Kassim Majaliwa akiagiza kukamatwa kwao.

Inasubiriwa kuona iwapo wataachiliwa huru na hatua itakayochukuliwa kuhusu fedha walizokusanya kwa lengo la kufadhili uokoaji na kusaidia waathiriwa wa mkasa wa Kariakoo.

Share This Article