Diddy ataka mahakama izuie wahusika wa kesi dhidi yake kuizungumzia hadharani

Marion Bosire
2 Min Read
P Diddy

Mawakili wa mwanamuziki aliye kizuizini P Diddy wameomba jaji atoe maagizo ya kuzuia wahusika wa kesi dhidi yake kuizungumzia nje ya mahakama.

Mawakili hao walitaja shahidi mmoja wa kesi hiyo kwa jina Courtney Burgess ambaye amekuwa akizungumza na wanahabari nje ya mahakama.

Burgess aliambia wanahabari kwamba anamiliki video zinazoonyesha Diddy akiwa anajihusisha katika ngono na watu maarufu wapatao wanane.

Video hizo ni kutoka kwenye baadhi ya sherehe ambazo Diddy alikuwa akiandaa kwa ajili ya ngono, na kulingana na Burgess, baadhi ya watu hao maarufu walikuwa na umri wa chini ya miaka 18.

Ombi hilo la mawakili wa Diddy liliwasilishwa Jumapili Novemba 3, 2024 na walitaka lishughulikiwe kwa haraka, wakisema madai ya Courtney sio ya kweli na yanalenga tu kumchafulia jina mteja wao.

Wanasheria hao wanahisi kwamba kwa kukosa kuchukulia madai kama hayo kuwa kashfa ya unyang’anyi, serikali inawezesha njama ya mitandaoni na kuifanya iwe vigumu kwa mteja wao kupata haki mahakamani.

Serikali ya Marekani imekuwa ikimchunguza Diddy kwa muda wa mwaka mmoja kulingana na mawakili wake ambao wanadai kwamba inafahamu kwamba sherehe anazodaiwa kuandaa za ngono hazikuhusisha wanaume au watoto.

Diddy alikamatwa mwezi Septemba mwaka huu wa 2024 kutokana na madai ya kuhusika katika njama ya uhalifu, ulanguzi wa binadamu ambao walilazimishwa kuhusika katika ngono, ulaghai na usafirishaji wa watu ili kuwahusisha katika ngono.

Anazuiliwa katika jela ya Brooklyn akisubiri kesi yake na kesi kadhaa zimewasilishwa mahakamani dhidi yake tangu alipokamatwa.

Share This Article