Kesi dhidi ya mwanamuziki na mfanyabiashara Sean Diddy Combs zinazidi kuongezeka kila kuchao na sasa analaumiwa kwa kulawiti mtoto mvulana wa miaka 10 mwaka 2005.
Mlalamishi ambaye jina lake limebanwa mkazi wa California anasema alikuwa akidhamiria kuwa mwanamuziki na mwigizaji wakati mshauri aliyekodiwa na wazazi wake alimpangia majaribio na Combs kwenye hoteli moja jijini New York.
Aliambia Combs kwamba angefanya lolote kuwa nyota wakati wa mkutano huo wa majaribio ambapo alipatiwa kinywaji kilichokuwa kimetiwa dawa akamsukuma na kumlazimisha afanye vitendo vya kingono.
Baadaye alipoteza fahamu na alipoamka akapata suruali yake imefunguliwa ambapo alilia na kuomba kuona wazazi wake.
Combs alimtishia akisema kwamba angemuumiza vibaya iwapo angesimulia kilichotokea.
Kesi hiyo ni moja kati ya mbili zilizowasilishwa mahakamani jana Jumatatu katika mahakama moja huko Manhattan, New York na wakili Tony Buzbee.
Diddy ambaye anazuiliwa na maafisa wa polisi anakabiliwa na kesi zinazohusiana na unyanyasaji wa kingono zipatazo 24 na zinazidi kuongezeka.
Buzbee alisema anawakilisha waathiriwa wa Diddy zaidi ya 150 na kufikia sasa amewasilisha kesi 17 dhidi ya Combs.
Kesi ya pili iliyowasilishwa jana ni ya jamaa anayesema alikuwa na umri wa miaka 17 pekee alipokwenda kufanya majaribio ya kujiunga na onyesho la uninga kwa jina “Making the Band”.
Kipindi hicho kilikuwa cha Diddy na mlalamishi anasema Diddy mwenyewe na mlinzi wake walimnyanyasa kingono mwaka 2008.
Mawakili wa Diddy hata hivyo wamepuuza kesi hizo wakisema wakili anayehusika anataka tu kuangaziwa kwenye vyombo vya habari na wala hajajitolea kutafuta ukweli.
Katika taarifa mawakili hao wamesema kwamba mahakamani ni ukweli utashinda. Ukweli huo wanasema ni kwamba Combs hakuwahi kunyanyasa yeyote kingono iwe ni mwanaume au mwanamke, mtoto au mtu mzima.
Diddy wa umri wa miaka 54, alikanusha mashtaka ya jinai ya ulanguzi wa binadamu kwa lengo la kuwatumia kingono katika mahakama ya Manhattan, ambapo anakabiliwa na mashtaka hayo.
Viongozi wa mashtaka wanamlaumu kwa kile wanachosema ni kulazimisha wanaume, wanawake na hata watoto kushiriki ngono bila kupenda huku akiwahonga au kuwatishia ili wasiseme.
Amekuwa katika jela huko Brooklyn kwa wiki sita sasa baada ya ombi la kuachiliwa kwa dhamana kukataliwa mara mbili na sasa amekata rufaa kuhusu kuzuiliwa.