Diddy adaiwa kujaribu kushawishi mashahidi na waamuzi

Marion Bosire
2 Min Read

P Diddy anadaiwa kujaribu kushawishi mashahidi na wanachama wa kundi la waamuzi katika kesi yake akiwa kizuizini.

Maafisa wa polisi walitekeleza msako kwenye seli ya mwanamuziki huyo mwisho wa mwezi jana na kutwaa vitu ambavyo wakili na mteja wake wanakubaliwa kuwa navyo na kuvitoa kwa waendesha mashtaka.

Haya ni kulingana na wakili wa Diddy aitwaye Marc Agnifilo.

Sasa imebainika kwamba Diddy alitumia njia zisizokubalika gerezani za mawasiliano kuwafikia mashahidi na waamuzi wa kesi yake.

Njia hizo ni pamoja na kutumia alama za siri za kutumia simu za wafungwa wengine kupiga simu kwa watu watatu mara moja na kutuma jumbe.

Waendesha mashtaka wanasema kwamba mwanamuziki huyo anayezuiliwa kwa tuhuma za ulanguzi wa watu ili kuwatumia kingono, alijaribu kuvuruga uchunguzi dhidi yake.

Viongozi hao wa mashtaka wanatofautiana na Agnifilo kuhusu kilichopatikana kwenye seli ya mteja wake na kukanusha madai ya kutwaa stakabadhi zake.

Wanasema waliotekeleza msako walipapasa folda iliyokuwa na stakabadhi hizo na walipohisi haikuwa na chochote kisichoruhusiwa wakaiweka kando.

Walipiga picha kitabu chake cha kuandika pamoja na kile cha anwani kisha wakaondoka kwenye seli hiyo.

Kulingana na maafisa hao, msako huo ulipangwa vilivyo kabla ya kutekelezwa na haukulenga Diddy au mfungwa mwingine bali ulilenga kuhakikisha usalama wa wahudumu wa gereza.

Agnifilo hata hivyo anaamini kwamba maafisa hao walichukua stakabadhi zilizo na deta kuhusu mkakati wao wa kushughulikia kesi ya Diddy.

Anataka kikao kiandaliwe cha wahusika wote ili kufahamu yaliyojiri wakati wa msako huo kwenye seli ya mteja wake.

Website |  + posts
Share This Article