Diamond Platnumz amezungumzia tetesi zilizosambaa awali kwamba alimtelekeza meneja wake wa muda mrefu Mkubwa fella ambaye anaugua.
Akizungumza kwenye kipindi cha Exclusive cha Lil Ommy ambapo alikuwa akihojiwa, Diamond alielezea kwamba yeye ndiye alikuwa msaidizi wa kwanza wa Fella aliposikia anaugua.
Msanii huyo alitanguliza kwa kusema kwamba anatambua mchango wa Mkubwa Fella katika maisha yake na hivyo hawezi, kuwa mpuuzi kiasi cha kukosa kumsaidia.
“Sio kweli wanachokisema, mi nilipopata taarifa kwamba Mkubwa anaumwa, ni mimi nilienda nikamkuta yuko hospitali moja ya Temeke sijui Mbagala, nikashauri tumpeleke hospitali kubwa zaidi,” alijitetea Diamond.
Aliendelea kusema jinsi meneja wake mwingine Babu Tale alivyoshauri wampeleke Mkubwa katika hospitali ya Muhimbili ambapo walipatiwa rufaa akaamua kumpeleka Hospitali ya TMJ huko Mikocheni na akagharamia matibabu.
Baadaye alipendekeza kwamba Mkubwa Fella apelekwe India kwa matibabu bora zaidi iwapo madaktari wangeruhusu. Alifanikiwa na akagharamia safari hiyo pamoja na matibabu.
Anasema kilichomfanya asonge nyuma katika suala zima la kuugua kwa Mkubwa Fella ni maneno aliyoambiwa yaliyosemwa na mke wa Mkubwa fella.
“Mkewe alisema kwamba mimi nasababisha watu wasimsaidie Fella, wakiamini kwamba mimi namaliza kila kitu,” alisema Diamond akifafanua kwamba ilibidiajitoe na kuweka wakala wake katika suala la kumhudumia Fella.
Anasema alifungua kundi kwenye Whatsapp na kumweka Fumbwe kama msimamizi na kumtaka alipie kila kitu ambacho kingehitajika. Alimweka pia meneja wa uendeshaji wa Wasafi Media kuwa wakala wake humo.
Tetesi za Diamond kukosa kumsaidia Mkubwa Fella zilijiri mwezi Januari mwaka huu wa 2026, wakati mke wake alijitokeza kuomba usaidizi.