Dereva wa lori alichomeka hadi kufa Jumatano asubuhi baada ya kuhusika kwenye ajali katika eneo la Sikata kwenye barabara kuu ya kutoka Webuye kuelekea Malaba.
Lori la kubebea mafuta alilokuwa akiendesha linaripotiwa kupoteza mwelekeo, kugonga mtambo wa transfoma na kuwaka moto. Juhudi za kumwokoa ziligonga mwamba kwani alikuwa amekwama.
Kamanda wa polisi katika kaunti ya Bungoma Francis Kooli alithibitisha kisa hicho akisema dereva huyo alikuwa akijaribu kukwepa kugonga gari la abiria na akaishia kugonga transfoma.
Kwingineko, watu 29 wanapokea matibabu katika hospitali ya misheni ya Kakuma baada ya dereva wa basi walimokuwa wakisafiria kupoteza mwelekeo na kuondoka barabarani gurudumu lilipopasuka.
Kamanda wa polisi katika eneo la Turkana Magharibi Richard Moracha alithibitisha kisa hicho akielezea kwamba basi hilo lilikuwa linaelekea Kitale ajali ilipotokea.
Ripoti yake Florence Masha