Demi Moore asema Bruce Willis yuko sawa

Marion Bosire
1 Min Read

Mwigizaji wa Marekani Demi Moore amesema kwamba aliyekuwa mume wake Bruce Willis ambaye anaugua ugonjwa wa ‘dementia’ yuko imara.

Alikuwa akizungumza kwenye mahojiano na mwigizaji mwenza Drew Barrymore kwenye kipindi chake cha mahojiano almaarufu “The Drew Barrymore Show”.

Drew ndiye aliuliza anavyoendelea Willis, ambapo Demi alielezea kwamba kila akisafiri hadi Los Angeles anajitahidi sana kutenga muda wa kumwona mume wake wa zamani.

Willis alithibitishwa kuugua ugonjwa huo mwezi Machi mwaka 2022 na mwaka uliofuata, familia yake ikatangaza kwamba amelazimika kuacha uigizaji.

Demi Moore alikuwa kwenye ndoa na Willis kati ya mwaka 1987 na mwaka 2000, na walibarikiwa na watoto watatu wa kike ambao ni Rumer wa umri wa miaka 36, Scout wa umri wa miaka 33 na Tallulah wa miaka 30.

Willis kwa sasa yuko kwenye ndoa na Emma Heming Willis, lakini bado Demi Moore anamjali akisema kwamba anakumbuka vyema maisha mazuri waliyoishi wakiwa kwenye ndoa.

Share This Article