Idara ya maafisa wa polisi wa makosa ya jinai, DCI imeelezea wasiwasi wake kufuatia kuongezeka kwa visa vya ulaghai wa fedha kupitia mitandao.
Kulingana na idara hiyo, Wakenya wengi wanahadaiwa kujiunga na uwekezaji kupitia mitandaoni, ambapo hulaghaiwa fedha zao.
Kupitia taarifa kwa mtandao wa X, DCI ilisema imeshuhudia ongezeko la malalamishi ya watu kulaghaiwa kupitia mitandaoni na kupoteza fedha nyingi.
Kitengo hicho kilisema maafisa wake wanachunguza visa kadha ambapo wawekezaji wamelaghaiwa fedha nyingi.
Aidha DCI iliwatahadharisha Wakenya wanaopania kuwekeza fedha mtandaoni almaarufu Cryptocurrency kubaini uhalali wa mitandao hiyo kupitia halmashauri ya masoko ya hisa, CMA na halmashauri ya mawasiliano nchini, CA.
“Tunawatahadharisha Wakenya na mtu mwingine yeyote dhidi ya uwekezaji wa kidijitali, hakikisha umebainisha iwapo uwekezaji huo umeidhinishwa na halmashauri ya masoko ya hisa na halmashauri ya mawasiliano nchini CA,” ilisema DCI kupitia taarifa
Kitengo cha DCI kilisema tamaa ya kujipatia faida kubwa huwafanya watu wengi kulaghaiwa kupitia mitandao.
Wananchi wametakiwa kupiga ripoti kwa idara ya DCI kumhusu yeyote anayewalaghai watu kupitia uwekezaji huo wa kidijitali kupitia nambari isiyotozwa malipo 0800722203.