DCI: Tuju hakutekwa nyara, alijifungia nyumbani kwake

Ripoti za Tuju kutekwa nyara na watu wasiojulikana mtaani Karen ziliibuka juzi Jumamosi. Mbunge huyo wa zamani wa Rarieda amejitokeza hii leo akisema alienda mafichoni akihofia maisha yake.

Martin Mwanje
2 Min Read
Mohamed Amin - Mkurugenzi wa DCI

Idara ya Upelelezi wa Jinai, DCI imesema Waziri wa zamani Raphael Tuju alikuwa nyumbani kwake muda wote yalipozuka madai kuwa ametekwa nyara. 

Mkurugenzi wa idara hiyo Mohamed Amin anasema mbunge huyo alizima simu majira ya saa 12:18 ili kusingizia kuwa ametekwa nyara.

Hata hivyo, DCI inasema uchambuzi wao wa kina, ikiwa ni pamoja na data za simu ya mbunge huyo wa zamani wa Rarieda zilionyesha alikuwa nyumbani kwake.

Amin amelaani hulka ya watu fulani kujiteka nyara na kisha kuwalimbikizia maafisa wa polisi lawama.

“Huduma ya Taifa ya Polisi itafuatilia tukio hili na matukio mengine sawia kikamilifu kwa mujibu wa sheria. Tumesimama kidete kuhakikisha majaribio ya kimakusudi ya kuwapotosha Wakenya, kubadhiri rasilimali za polisi na kudhoofisha imani katika asasi zetu za umma yanachunguzwa kikamilifu na wahusika kuwajibishwa,” alisema Amin wakati akiwahutubia wanahabari dakika chache baada ya Tuju kujitokeza.

Mkurugenzi huyo aliongeza kuwa Tuju alizuiliwa katika kituo cha polisi cha Karen ili kuandikisha taarifa kuhusiana na tukio hilo.

Akizungumza katika eneo la Tiaty, Waziri wa Usalama wa Taifa Kipchumba Murkomen pia alilaani kitendo cha Tuju kujiteka nyara akionya kuwa vitendo kama hivyo vinapaswa kukabiliwa vilivyo.

“Mtu hawezi kuchochea umma na kusababisha purukushani baada ya kujiteka nyara mwenyewe,” alisema Murkomen.

Aliitaka idara ya mahakama kuwa macho inaposhughulikia kesi za utekaji nyara wa kujisingizia na kuuonya upinzani dhidi ya kuingiza siasa katika masuala ya usalama.

Tuju alijitokeza hadharani hii leo na kusema kwamba alienda mafichoni akihofia maisha yake baada ya kuandamwa na watu wasiojulikana.

Ripoti za “kutekwa nyara” kwake ziliibuka juzi Jumamosi katika hatua iliyosababisha miito kwa mamlaka kufanya kila ziwezalo kuhakikisha anapatikana.

Wengi walihusisha masaibu ya Tuju na mzozo wa mali yake ya mamilioni ya pesa iliyopo kwenye barabara ya Ngong.

 

Share This Article