Dawood atetea hatua yake ya kuunga mkono mswada wa fedha

Marion Bosire
1 Min Read

Mbunge wa eneo la Imenti Kaskazini Rahim Dawood ametetea hatua yake ya kupiga kura bungeni kuunga mkono mswada wa fedha wa mwaka 2024 uliozua utata kote nchini.

Akizungumza huko Meru jana, mbunge huyo alielezea kwamba alihisi ni wazo zuri kuunga mkono mswada huo ambao ulipendekeza ushuru zaidi kwani ungesababisha eneo bunge lake na kaunti ya Meru kupata miradi ya maendeleo.

Kuhusu suala la kupunguza matumizi ya fedha serikalini, Rahim alisema ataunga mkono wazo la kupunguza mishahara ya wabunge na maseneta na kuondolewa kabisa kwa wadhifa wa Gavana.

Kulingana naye, kuondoa bunge la seneti, kupunguza maeneo bunge na mishahara ya wabunge pia ni wazo ambalo linaweza kutumiwa kupunguza matumizi ya fedha serikalini.

Mbunge huyo wa Imenti kaskazini alipongeza hatua iliyochukuliwa na Rais ya kupunguza idadi ya mawaziri na mashirika ya kiserikali akisema itasaidia pakubwa kupunguza matumizi ya fedha.

Mswada wa fedha wa mwaka 2024 ulipingwa vikali na wakenya huku wale wa kizazi cha Gen Z wakitekeleza maandamano kwa sababu hiyo hatua iliyosababisha Rais Ruto akose kuutia saini kuwa sheria.

Waandamanaji walitambua wabunge waliounga mkono mswada huo bungeni na wengi wamekuwa wakiwawajibisha kwa kukosa kuwapa fursa ya kuzungumza kwenye mikutano mashinani na hata makanisani.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *