Davido aonya waliomtaja kwenye utekaji nyara

Mmoja wa waliokamatwa kwa kushukiwa kuwa watekaji nyara alisema jina lake la utani ni Davido.

Marion Bosire
2 Min Read

Mwanamuziki wa Nigeria Davido ametoa onyo kali kwa wanahabari wa mitandaoni waliomtaja kwenye kisa fulani cha utekaji nyara.

Akaunti hiyo ilichapisha video ya watu watatu wanaodaiwa kuwa watekaji nyara na mmoja wao akajitambulisha kama Davido.

Watatu hao walikuwa wamekamatwa na wakazi wa eneo moja la Lagos na wanapotakiwa kujitambua, mmoja akasema anaitwa Ifeanyi mzaliwa wa jimbo la Anambra.

Kiongozi huyo wa kundi hilo aliendelea kusema kwamba jina lake la utani ni Davido na alikuwa amefika katika eneo hilo la makazi kwa ajili ya kuteka nyara.

Washukiwa wengine wawili walijitambulisha kama wazaliwa wa majimbo ya Kwara na Imo. Katika maelezo chini ya video hiyo, akaunti hiyo ya habari mitandaoni iliandika, “Davido na wengine wawili wakamatwa kwa utekaji nyara Lagos”.

Davido alichapisha video hiyo kwenye akaunti yake ya X pamoja na maelezo ambapo ametajwa akisema siku moja kisasi kitawafika wanaomharibia sifa.

Wanaoendesha akaunti hiyo waliamua kufuta taarifa hiyo kufuatia usemi wa Davido labda kama njia ya kujinusuru wasije wakachukuliwa hatua za kisheria.

Watu wengine maarufu nchini Nigeria ambao waliona chapisho hilo walitoa maoni yao akiwemo Tunde Ednut, aliyeshangaa ni kwa nini wamtaje nyota huyo wa muziki wakijua hahusiki kwa vyovyote.

Mwigizaji Juliet Ibrahim aliandika, “Hawa wanablogu hawaelewi uzito wa matendo yao wakati mwingine. Iwapo mtu aliye popote ulimwenguni atatafuta jina Davido mitandaoni, kitakachoonekana kwanza ni tangazo hilo lisilo la kweli.”

“Binti huyo aliendelea kusema kwamba usemi kama huo unaweza kuharibia watu maarufu fursa nyingi.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *