Mwigizaji Danny Trejo amesema kwa maoni yake, haoni iwapo Rais mteule wa Marekani Donald Trump atatekeleza ufurushaji wa wahamiaji wasio na stakabadhi halali.
Trejo anahisi kwamba serikali ya Marekani haina fedha za kutosha kutekeleza ufurushaji huo.
Ingawa hampendelei sana Trump, Trejo amesema hana tatizo na yeyote aliyempigia kura na kamwe hawezi kuelekeza yeyote kuhusu kiongozi wa kupigia kura.
Hata hivyo mwigizaji huyo ameahidi kujituma vilivyo kuhakikisha Gavana wa California Gavin Newsom anachaguliwa Rais wa Marekani mwaka 2028.
Danny amemtaka Trump akome kuingilia taifa la Mexico kwani nchi hiyo ina namna ya kipekee ya kulipiza kisasi.
Huku haya yakijiri, Trump na wote aliowateua kwa nyadhifa za uwaziri wanaonekana kumakinika na suala hilo la kufurusha wahamiaji haramu.
Taasisi za elimu, biashara na miji inajipanga kutafuta suluhisho katika usimamizi wa maeneo hayo iwapo Trump atatekeleza ufurushaji huo.
Lakini Danny anahisi kwamba shughuli kama hiyo ni ya kuharibu muda tu kwani hakuna mahali wahamiaji wanaenda kutoka Marekani.