Daniel Ebenyo Simiu amekuwa Mkenya wa kwanza kunyakua nishani katika makala ya mwaka huu ya mashindano ya Riadha Duniani yanayoendelea mjini Budapest Hungary.
Ebenyo amenyakua fedha katika fainali ya mita 10,000,wanaume Jumapili jioni akiziparakasa kwa dakika 27 sekunde 52 nukta 60.
Joshua Cheptegei wa Uganda amenyakua dhahabu ya fainali hiyo kwa mara ya tatu kwa mpigo akitumia dakika 27 sekunde 51 nukta 42,huku Selemon Barega wa Ethiopia akiridhia medali ya shaba kwa dakika 27 sekunde 52 nukta 72.
Matumaini ya Ferdinand Omanyala kunyakua nishani ya kwanza na kuwa Mkenya wa kwanza kushinda medali ya dunia katika mita 100,yaliyeyuka baada ya kuambulia nafasi ya 7 kwenye fainali kwa sekunde 10 nukta 07.
Bingwa wa dunia wa mita 200 katika mashindano ya Oregon mwaka uliopita Noah Lyles ameshinda dhahabu ya mita 100 akiweka muda muda wa kasi ulimwenguni wa sekunde 9 nukta 83,huku fedha ikinyakuliwa na Letsile Tebogo wa Botswana kwa sekunde 9 nukta 88 wakati Zharnel Hughes wa Uingereza akiridhia nishani ya shaba.