Daima kaeni chonjo, Mudavadi ayaambia mashirika ya kukabiliana na ufisadi

Martin Mwanje
2 Min Read

Mashirika ya kukabiliana na ufisadi nchini yametakiwa kuwa macho kila wakati ili kuongeza wajibu wao wa kuzuia uovu huo na hatua za kufanikisha vita dhidi ya ufisadi. 

Waziri Mwenye Mamlaka Makuu Musalia Mudavadi anasema ufisadi ni tishio kubwa kwa matamanio ya Wakenya na wakati umewadia wa kutokomeza kwa kuling’ata jinamizi hilo la sivyo jitihada za kuliangamiza zigeuke kuwa ngumu.

“Wakenya wamekuwa wakijiuliza kwa nini mizizi ya ufisadi inaenea licha ya mlipa kodi kutumia hela nyingi kugharimia shughuli za mashirika ya kukabiliana na ufisadi,” Mudavadi alisikitika.

“Utafiti unaashiria ufisadi unadunisha maendeleo na utoaji huduma kwa kuchepua rasilimali za maendeleo kuwa mafao ya kibinafsi ya watu wachache, kusababisha kupotea kwa kodi, kuongeza gharama ya kufanya biashara na hivyo kuzuia maendeleo.”

Ingawa serikali inajibidiisha kuboresha maisha ya Wakenya wengi ambao kwa sasa wameelemewa na gharama ya juu ya maisha, Mudavadi alilalama kuwa ufisadi unaendelea kuyumbisha ukuaji mkubwa wa uchumi unaotarajiwa.

“Vyote hivi vinafanya kazi ya utekelezaji wa sera na mipango ya serikali kuwa ngumu zaidi. Nina ujasiri wa kusema hili kwa sababu nimekuwa mwathiriwa wa ufisadi katika kubuni Ofisi ya Waziri Mwenye Mamlaka Makuu,” aliongeza Mudavadi.

Aliyasema hayo wakati wa uzinduzi wa mpango wa kimkakati wa mwaka  2023-2028 wa Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi, EACC uliofanyika katika Jumba la Mikutano ya Kimataifa la Kenyatta, KICC jijini Nairobi leo Jumanne.

Kulingana na Mudavadi, wale wote watakaopatikana wakijihusisha na ufisadi watakachukuliwa hatua kali chini ya uongozi wa Rais William Ruto.

Website |  + posts
Share This Article