Mchekeshaji wa mitandaoni Kennedy Odhiambo maarufu kama Crazy Kennar amezungumza kwa mara ya kwanza tangu ujumbe aliouweka kwenye akaunti zake kusababisha watu wahisi alikuwa akipitia changamoto.
Julai 4, 2023, Kennar aliandika kwenye akaunti zake za mitandao ya kijamii maneno haya, “Depression is Real” ishara kwamba alikuwa na msongo wa mawazo. Wengi walihusisha maneno hayo na kuondokewa kwa watu ambao amekuwa akishirikiana nao katika kuandaa video zake za vichekesho mitandaoni.
Siku hiyo hiyo, Yvonne Khisa mmoja wa waigizaji wenzake naye aliandika ujumbe wa kuzua hofu ya kusambaratika kwa kundi lao. Khisa aliandika, “Watu wabaya kujifanya kuwa waathiriwa ndilo jambo la kuchekesha sana.”
Dada mwingine kwa jina Wanjiru Africas ambaye amekuwa akiigiza na Kennar naye aliandika, “Wanaume wanaweza kukuacha jangwani bila hata maji. La wanaume watakuacha jangwani bila maji. Lakini ni siku nyingine ya kukukumbusha kwamba unafaa kupigania nafasi yako kwa vyovyote vile.”
Mwigizaji wa kiume ambaye alikuwa akishirikiana na Kennar anayefahamika kama Stano aliacha kufanya kazi naye mwezi Mei lakini akasema hawakukosana ila aliamua kufanya kazi peke yake.
Ujumbe wa Kennar siku ya leo ni wa kushukuru mashabiki, marafiki, wateja na jamaa ambao walichukua hatua ya kumjulia hali kila mara kwa muda ambao amekaa bila kutayarisha video zake kama kawaida.
Hakusema kilichokuwa kikimsibu ila alisema amekuwa akipokea jumbe kutoka kwa watu ambao wanapitia matatizo mengi na hawezi kuwasaidia yeye peke yake. Aliahidi kuendelea kuandaa video za kuwafanya watu watabasamu na akaomba wafuasi wake wazisambaze kwa wale ambao wanahitaji sababu ya kutabasamu.