COTU yampongeza Trump kwa kushinda uchaguzi Marekani

Martin Mwanje
1 Min Read
Donald Trump ashinda uchaguzi wa Marekani 2024.

Muungano wa Vyama vya Wafanyakazi nchini Kenya (COTU) umempongeza Donald Trump kwa kushinda uchaguzi wa urais nchini Marekani. 

Kupitia Katibu Mkuu Francis Atwoli, COTU inasema kuchaguliwa kwa Trump kuhudumu kama Rais wa 47 wa Marekani kumewadia wakati muhimu.

“Taarifa za kuchaguliwa kwa Trump kulipokelewa vyema na furaha kubwa na wafanyakazi nchini Kenya ikizingatiwa uhusiano mzuri uliopo kati ya Kenya na Marekani,” amsema Atwoli katika taarifa.

“Ni muhimu kukumbuka kuwa, nchi kote duniani zina mahitaji makubwa ya viongozi thabiti ambao pia ni wacha Mungu na wanaweza wakachukua uamuzi thabiti kuhusiana na masuala mbalimbali duniani. Kwa misingi hiyo, kuchaguliwa kwa Rais Trump siyo tu ushindi kwa ajili ya uthabiti duniani lakini pia mwanzo mpya wa uongozi mzuri na wa vitendo.”

Atwoli ameyasema hayo wakati mgombea wa chama cha Democrat Kamala Harris amekiri kushindwa kwenye uchaguzi huo na pia kumpongeza Trump kufuatia ushindi wake.

Harris ameahidi kuhakikisha mpito mzuri utakaopisha uongozi wa Trump akisema atamuunga mkono katika utenda kazi wake.

Rais wa zamani wa Marekani Barack Obama pia amempongeza Trump kufuatia ushindi wake.

 

 

 

 

Website |  + posts
Share This Article