COTU: Serikali ihakikishe usalama wa polisi watakaotumwa Haiti

Martin Mwanje
2 Min Read
Katibu Mkuu wa COTU Francis Atwoli

Serikali imetakiwa kushirikiana na washirika wake kama vile Marekani na Canada kuhakikisha usalama wa maafisa wa polisi watakaotumwa nchini Haiti ili kudhibiti usalama katika taifa hilo la Carribean.  

Umoja wa Mataifa tayari umeunga mkono pendekezo la Kenya la kuongoza kikosi cha kimataifa cha usalama nchini Haiti, kujibu ombi la Waziri Mkuu wa taifa hilo la kusaidiwa kurejesha utulivu.

“Ingawa serikali ya Kenya ina wajibu wa kimataifa wa kudumisha amani na usalama duniani kama mshirika mkuu chini ya mamlaka ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, tungependa kutoa wito kwa serikali kutahadhari zaidi ikiwa ni pamoja na kuhusisha washirika wetu ambao tayari wameunga mkono hatua kama hiyo kama vile Marekani na Canada ili kuhakikisha usalama wa maafisa wetu wa polisi amba watatekeleza wajibu muhimu wa kulinda maisha ya ndugu zetu nchini Haiti,” anasema Francis Atwoli, Katibu Mkuu wa COTU.

COTU inasema imepokea taarifa kutoka kwa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi vya Amerika (TUCA) likielezea mashaka makubwa kuhusiana na uamuzi wa serikali ya Kenya kutuma maafisa wa polisi 1,000 nchini Haiti.

“Maafisa wa polisi wa Kenya huenda wanaingia katika ‘vita vya magenge ya wahalifu’ nchini Haiti ikizingatiwa kuwa jitihada za awali kama hizo zilizochukuliwa na mataifa ya kigeni kutokomeza makundi hayo hazikuzaa matunda,” inasema TUCA katika taarifa yake kwa COTU.

Kwa upande wake, Atwoli pia ametoa wito kwa Marekani kufidia kujitolea kwa serikali ya Kenya kwa kuhakikisha maafisa wa polisi wa Kenya wana vifaa vinavyohitajika vya kuhamasisha amani na usalama wakati wakihakikisha usalama wao.

 

Share This Article