Clansman amshambulia Navio katika wimbo

Hii ni baada ya Navio na mlinzi wake kudaiwa kumshambulia Clansman katika sehemu ya burudani usiku.

Marion Bosire
1 Min Read
Chief Clansman

Mwanamuziki wa mtindo wa Hip Hop nchini Uganda Chief Clansman ameamua kutumia wimbo, kumshambulia mwanamuziki mwenza Navio kwa madai kwamba yeye na kundi lake walimshambulia katika eneo la burudani la 1420 jijini, Kampala.

Clansman alichapisha sauti ya wimbo huo katika akaunti yake ya mtandao wa X na kuandika, “Rapa fulani aliyetoka Chanel O alijaribu kinishambulia jana usiku akiwa na mlinzi wake na rafiki yake mnene”.

Aliendelea kuhimiza mwanamuziki huyo ambaye hakumtaja jina awe mkweli iwapo anataka wapigane lakini kwa sasa aende akaokote vipande vya shati lake.

Katika wimbo huo Clansman anasimulia kuhusu ugumu aliopitia awali kama vile kufiwa na mama akiwa na umri wa miaka 17 pekee huku akimtaja Navio kuwa “mwana wa mama”.

MC Alan King, ambaye huenda alishuhudia kisa hicho cha makabiliano cha Juni 20, 2025 aliandika haya kwenye akaunti yake ya X, “Lakini ni nini kinaendelea katika tasnia ya hip-hop??? Jana usiku katika klabu cha 1420, Navio na mlinzi wake walimshambulia Chief Clansman”.

Alan King aliendelea kusema jinsi makonde yalirushwa, shati la Navi likachanwa vipande vipande na damu ya Clansman ikatapakaa.

Navio hata hivyo hajatoa taarifa kuhusu tukio hilo.

 

Website |  + posts
Share This Article