Rais wa chama cha wasanii wa muziki nchini Uganda -UMA, Cindy Sanyu, ametangaza nia yake ya kuwasilisha malalamiko rasmi kwa Rais Yoweri Museveni kuhusu hulka ya serikali kudhoofisha taaluma za wanamuziki wanaoamua pia kujihusisha na siasa za upinzani.
Mwanamuziki huyo amesema atazungumzia suala hilo katika kikao kijacho kati ya chama hicho cha wanamuziki na Rais Museveni.
“Hivi karibuni tutakuwa na kikao kama viongozi wa chama cha wasanii muziki wa Uganda na Rais Yoweri Museveni, na hili ni jambo nitakalolizungumzia,” alisema.
“Nitamwuliza kama kuna uwezekano wa kutofautisha kati ya taaluma ya muziki na taaluma ya kisiasa ya mtu.”
Cindy alionyesha masikitiko yake kwamba rafiki yake na msanii mwenzake Bobi Wine hakuweza kuungana naye jukwaani katika tamasha lake.
“Ninamkosa sana, hasa kwa kuwa tuna wimbo wa pamoja,” alisema.
“Kwenye tamasha langu, ingekuwa ni furaha kubwa kumuona akipanda jukwaani kama Bobi Wine, siyo kama Kyagulanyi, kiongozi wa kisiasa.”