Matumaini ya timu ya taifa ya soka ya Kenya – Harambee Stars – kufuzu kwa Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza, yameambulia pakavu baada ya kuzimwa nyumbani uwanjani Nyayo, kufuatia kipigo cha 2-1 na wageni Panthers kutoka Gabon.
Pierre Emrick Aubameyang, alipachika magoli yote kwa wageni kunako dakika ya 16 na 52 kupitia penati huku nahodha Michael Olunga akifunga la kufutia machozi kwa Harambee Stars dakika ya 62.
Kenya ilipoteza nafasi chungu nzima za kufunga magoli huku safu ya ulinzi ikifanya makosa mengi.
Ushinde huo unamaanisha kuwa tayari Kenya wamebanduliwa kwa safari ya kufuzu kwa Kombe la dunia mwaka ujao hata ikiwa watashinda mechi zote nne zilizosalia.
Harambee Stars watawaalika Gambia mwezi Septemba 3 na kuwaalika pia ushelisheli wiki moja baadaye.
Ilikuwa mechi ya kwanza ya timu ya taifa ya Kenya kucheza mbele ya uwanja uliojaa mashabiki wa nyumbani tangu miaka sita iliyopita.
Kenya watazuru Burundi na Ivory Coast katika mechi mbili za mwisho mwezi Oktoba mwaka huu.
Gabon wanaongoza kundi F kwa alama 15, pointi 2 zaidi ya mabingwa wa Afrika, Ivory Coast, ambao watawaalika Gambia kesho.