Chui wa Congo wasalimu amri mbele Simba wa Uingereza

Uingereza itamenyana na waandalizi wenza Mexico katika uwanja wa Mexico City Julai 7 kuwania tiketi ya kufuzu kwa robo fainali.

Dismas Otuke
1 Min Read

The Leopards ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC ilijikaza kisabuni ikaongoza kipindi cha kwanza, lakini ikapigwa laza na Three Lions ya Uingereza katika mechi ya awamu ya 32 ya Kombe la Dunia katika uchanjaa wa Atlanta nchini Marekani.

Brian Cipenga aliwaweka Chui wa Congo uongozini kunako dakika ya saba na wakafanikiwa kulinda goli hilo hadi mwishoni mwa kipindi cha kwanza.

Kipa wa Congo Mpasi Nzau alichangia pakubwa kuwaweka uongozini akipangua matobwe kadhaa ya Waingereza, huku pia safu ya nyuma ikijihami vilivyo.

Shinikizo kubwa na mashambulizi ya Waingereza yalizaa matunda katika dakika 75 baada ya Anthony Gordon kumdokolea pasi Harry Kane aliyesawazisha kabla ya kupachika la ushindi dakika 11 baadaye.

Uingereza itamenyana na waandalizi wenza Mexico katika uwanja wa Mexico City Julai 7 kuwania tiketi ya kufuzu kwa robo fainali.

Share This Article