Mwimbaji wa nyimbo za injili nchini Tanzania Christina Shusho amevunja kimya chake kuhusu video ambazo zimekuwa zikisambazwa ambapo anaonekana akizungumza kuhusu ndoa yake kwenye mahojiano.
Katika video hizo anaelezea kwamba aliolewa akiwa na umri wa miaka 19 pekee kwa sababu alikuwa mrembo na wazazi wake walihofia usalama wake na hivyo wakaamua kumwoza.
Mwimbaji huyo aliashiria pia utengano na mume wake ili aweze kumtumikia Mungu ipasavyo. Video hiyo imezua gumzo mitandaoni na kusababisha Christina kutoa taarifa.
Kwenye taarifa hiyo amezungumzia wanahabari wanaomtafuta kwa ajili ya kuweka mambo wazi akisema wakati utakapowadia atawaambia ukweli uliopo.
Video hizo anasema ni za mahojiano aliyoyafanya mwaka 2020 na mwaka 2022 na kwamba amewashtaki mahakamani wote ambao wanazitumia na kutumia picha zake kusambaza habari wasizozijua kwa undani.
Aliahidi pia kuweka paruwanja masuala yote kuhusu ndoa yake kwani anaamini kwamba ukweli siku zote humweka mtu huru. Christina aliolewa na John Shusho ambaye ni mhubiri na wana watoto watatu na sasa inasubiriwa kufahamu iwapo bado wako pamoja au wametengana.
Minong’ono kuhusu ndoa ya mwimbaji Shusho ilichochewa zaidi na hatua yake ya kufungua kanisa jingine ilhali mume wake ana kanisa. Ilitarajiwa kwamba wawili hao wangehudumu kwenye kanisa moja.