Chipukizi wa Kenya kuelekea Peru kwa mashindano ya Riadha ya Dunia

Dismas Otuke
1 Min Read

Kikosi cha timu ya Kenya kwa wanariadha wasiozidi umri wa miaka 20 kitaondoka nchini Jumamosi usiku kwenda mjini Lima Peru, kushiriki makala ya 20 ya mashindano ya Dunia.

Mashindano hayo yataandaliwa kati ya Agosti 27 na 31, yakiwashirikisha wanariadha zaidi ya 900 kutoka mataifa 135.

Timu hiyo yenye wanariadha 21 wanaume 11 na wanawake 10 itasafiri kwa ndege ya KLM, kundi la kwanza likiondoka saa tano kasoro dakika 10 usiku na kundi la mwisho muda mfupi kabla ya usiku wa manane.

Wanariadha hao ambao  wamekuwa kwenye kambi ya mazoezi ya zaidi ya majuma mawili katika uwanja wa Kasarani walikabidhiwa bendera ya taifa na waziri wa Michezo Kipchumba Murkomen.

Kenya chini ya Kocha Robert Ng’isirei itatea mataji matatu ya iliyotwaa katika makala ya Cali,Colombia ya mita 1500 wanaume,mita 3,000 na 3,000 kuruka viunzi na maji kwa wanawake.

Washindi wa medali katika makala ya mwaka huu ya mashindano ya Afrika Edmund Serem,aliyeshinda fedha ya 3,000 kuruka viunzi na maji na Sarah Moraa aliyenyakua dhahabu ya mita 800 watakongeza mchakato wa kusaka medali kwa chipukizi hao mjini Lima.

Zaidi ya wanariadha 900 kutoka mataifa 135 watashiriki mashidnano hayo ya siku tano yanayoandaliwa Amerika Kusini kwa mara ya pili mtawalia.

Share This Article