China imeahidi kuziunga mkono kampuni zinazoendeshea shughuli zake nchini Kenya katika utekelezaji wa miradi ya miundombinu ikiwa ni pamoja na barabara, reli, usafiri wa anga na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano, ICT.
Li Xi, mwanachama mwandamizi wa ofisi ya kisiasa ya Chama cha Kikomunisti cha China alisema nchini yake inatambua Ajenda ya Mabadiliko ya Kiuchumi kuanzia Chini hadi Juu (BETA) ya Rais William Ruto.
Alisema ajenda hiyo inalenga kuchochea ukuaji wa uchumi kutokea tabaka la chini la nchi hiyo.
“Mpango wa uchumi wa kuanzia chini hadi juu unawiana na imani ya Rais Xi Jinping na tutaunga mkono mipango yako”, alisema Li Xi, alipokutana na Rais Ruto anayefanya ziara rasmi nchini China.
Miongoni mwa miradi ambayo China inalenga kuwekeza nchini Kenya ni pamoja na ujenzi wa barabara, upanuzi wa reli ya SGR, sekta ya ICT na kuvifanya viwanja vya ndege kuwa vya kisasa.
“China na Kenya zina ndoto sawa ya kuangamiza ufukara kupitia mabadiliko ya kijamii na kiuchumi kuanzia chini na tumetambua nyanja ambazo tunaweza tukaziunga mkono ili kufikia maono haya,” alisema Li.
Rais Ruto aliuambia ujumbe wa China kuwa Kenya inabuni mazingira mwafaka ya ufanyaji biashara na kuwaalika wawekezaji Wachina kuwekeza katika kile alichokielezea kuwa fursa nyingi zilizopo katika sekta mbalimbali nchini.
“Tuna fursa mbalimbali katika miundombonu, ICT, kilimo na nishati na niwawaomba kuwekeza fedha zenu katika sekta hizo”, alisema Rais Ruto.
Rais Ruto pia atahudhuria Kongamano la 3 la Ukanda Mmoja, Njia Moja kwa ajili ya Ushirikiano wa Kimataifa litakalofanyika jijini Beijing.
“Kongamano hilo litakuwa fursa ya kujadili nyanja mbalimbali za ushirikiano ambazo ni za manufaa ya pande mbili kati ya nchi zetu“, alisema Rais Ruto.
Waziri wa Uchukuzi Kipchumba Murkomen alihudhuria mkutano huo.